Samatta baada ya kuumia bega uwanjani.
BAADHI ya madaktari wa timu za Ligi Kuu hawana taaluma hali inayosababisha wachezaji kushuka viwango mapema kutokana na kuwa majeruhi muda mrefu.
Mmoja wa madaktari ambaye hakutaka jina lake kuandikwa kwenye gazeti, alisema fani ya udaktari wa timu za Ligi Kuu imevamiwa na madaktari makanjanja.
"Inashangaza sana, daktari anayejua kutoa dawa tu ya kutuliza maumivu, leo anapewa jukumu la kuwa daktari wa timu. Hii siyo sahihi kabisa," alisema daktari huyo.
"Hivi daktari wa aina hiyo anapokutana na tukio la kuanguka kama lililomkuta Fabrice Muamba anaweza kufanya lolote la maana kuokoa maisha ya mchezaji," alihoji.
Alisema haishangazi kuona timu nyingi za Ligi Kuu zikiwa na wachezaji wengi majeruhi kutokana na udhaifu wa kitaaluma kwa madaktari waliowaajiri.
Daktari huyo alisema, ukindoa timu za Mtibwa, Kagera, Simba, Azam timu zingine zilizobaki zimekuwa na majeruhi wengi msimu mzima.
"Timu hizi zina madaktari wenye taaluma, wanajua kazi zao. Sina hakika timu zingine kama zina madaktari kama hao," alisema.
Aliongeza: "Kwa soka la Tanzania, ni kawaida mchezaji kucheza vizuri msimu wa kwanza, lakini akipata majeruhi kidogo msimu unaofuata anapotea."
"TFF ifuatilie Wizara ya Afya ili kufahamu kama madaktari wa timu wanatambuliwa na wizara kutokana na kukidhi viwango vya taaluma ya michezo."
Kuhusu vigezo vinavyokubalika, alisema daktari ni lazima awe na cheti cha 'Assitant Clinical Officer', 'Second Clinical Officer', 'Assistant Medical Officer' au 'Medical Officer' na kuendelea.
Akizungumzia suala hilo Katibu mkuu wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mwanandi Mwankemwa alisema tatizo la madaktari 'kanjanja' lipo na wameshaanza kulifanyia kazi.
"Madaktari wa klabu wengi ni wanachama wa Tasma (Chama cha Madaktari Tanzania), lakini siyo wote wenye vigezo vinavyokubalika,' alisema Mwankemwa.
"Tatizo kubwa la madaktari feki linatokana na klabu kushindwa kuwalipa mshahara madaktari wenye taalamu kwa vile wanahitaji mishahara mikubwa," alisisitiza Mwankemwa.