Yako mambo mengi madogo madogo ambayo watu hutenda na kuleta mabadiliko.
Lakini, kila wakati lazima pawepo msukumo ili kufanikiwa, iwe katika
nyanja za elimu, afya bora, mazingira safi na mengineyo.
Hali ya mazingira wakati huu ina umuhimu zaidi kuliko
ilivyokuwa siku za nyuma kutokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na
athari zake zisizofikirika katika maendeleo ya binadamu.
Wakati wanasayansi wanajadili uhusiano kati ya uunguzaji
wa mafuta ya asilimwamba, kuongezeka kwa hewa ukaa na kupanda kwa
halijoto duniani, Watanzania wanahitajika kuchukua hatua za haraka
kurekebisha uharibifu mkubwa wa mazingira yao.
Ni zaidi ya miongo miwili tangu mfumo wa siasa za vyama
vingi ulipoanzishwa Tanzania, lakini raia wa nchi hii bado si wepesi
kuanzisha au kujiunga na vikundi vya hiari ambavyo vinaweza kuharakisha
maendeleo na kuepusha mgogoro wa kimazingira ambao unaweza kutokea.
Shauku iliyoambatana na ushindi wa jumuiya za kiraia
katika kuanzisha vyama vya siasa imefifia. Hata baadhi ya vyama
vimepotea hivyo hivyo.
Lakini bado watu wanalalamika kuhusu ongezeko la
umasikini; elimu duni; uhaba wa huduma bora za afya; unyanyasaji wa
wanawake na watoto; ubaguzi wa kijinsia katika taratibu za kufanya
maamuzi; ukosefu wa makazi bora; hali duni ya huduma za usafi wa
mazingira na mambo mengine mengi katika mlolongo wa mapungufu katika
maisha ya kila siku Tanzania.
Wakulima wadogo hawana imani tena na vyama vya ushirika.
Katika mikoa ambapo vyama hivyo vilikuwa mhimili wa maendeleo kutokana
na uuzaji wa mazao ya biashara hali imerudi nyuma baada ya kushuka kwa
bei za mazao pamoja na uzalishaji.
Hali ni hiyo hiyo mijini ambako vyama vya ushirika wa
walaji vilikuwa vimestawi kutokana na mafanikio ya kutetea haki za
walaji na kuwasogezea bidhaa karibu. Wakati walaji wakiongezeka kila
mwaka, vyama hivyo vimetoweka.
Mvua kubwa ziliponyesha wiki ya kwanza ya mwezi huu wa
Mei katika ukanda wa pwani na kusababisha uharibifu uliotokana na
mafuriko Dar es Salaam na Zanzibar, watu wengi walianza kutafakari
wakijiuliza ni kitu gani kimevuruga mwenendo wa maisha. Zama zimepita
ambapo jumuia zilijitoa kukabili changamoto kama hizo kabla ya kuomba
msaada kutoka nje.
Kwa kiwango kikubwa mafuriko ya sasa ni changamoto kwa serikali kufanya matengenezo, kupanga na kujenga miundombinu inayofaa.
Maafisa wa serikali wamewaambia wakazi wa mabondeni
ambayo hufurika wakati wa mvua wajijue wenyewe, kwa sababu mara kwa mara
wamekaidi kufuata ushauri wa kuhamia sehemu za miinuko. Lakini
waathirika pamoja na familia zao wanalia wapate msaada ambao
haupatikani.
Wiki moja kabla ya mafuriko, wakazi wa mitaa ya Avocado,
Kawe Beach and Mzimuni wilayani Kinondoni katika jiji la Dar es Salaam
walitangazwa katika taarifa za televisheni kuwa ni mfano wa watu
wanaojali kupendezesha mazingira yao.
Wana nia thabiti kutunza usafi wa mitaa, siyo tu kwa
kuondoa taka lakini pia kuzuia madawa ya kulevya na uhalifu, vitu
ambavyo vimeharibu sifa za maeneo mengi ya mijini na kuwanyima wananchi
raha ya kujisikia kuwa na jumuiya zao wenyewe.
Wakati huo, mbunge wa jimbo la Ludewa kusini mwa
Tanzania amefaulu kuwaunganisha wananchi, bila kujali vyama vyao vya
siasa, wafanye kazi bila malipo kukamilisha mradi wa usambazaji umeme
vijijini. Kwa kuwashawishi, ameweza kuwaongoza wafanye kazi ambayo
italeta mabadiliko ya kudumu katika maisha baada ya vijiji vyao kupata
umeme kutoka gridi ya taifa.
Hivyo basi kwa nini vikundi vya kiraia vilivyokuwa na
mwamko zamani vimefifia baada ya demokrasia kuimarishwa? Kila mtu
angetarajia kuona mwamko wa kiraia umeshamiri badala ya kufifia katika
mfumo mpya wa kidemokrasia.
Kwa bahati mbaya, sivyo ilivyo. Jumuia nyingi zinakosa
viongozi wa kuwashikia mwenge na kuwahamasisha ili watende mambo ambayo
yataiwezesha nchi hii iwe mahali bora pa kuishi.
Mwandishi: Anaclet Rweyagura/ DW Dar es Salaam
Mhariri: Daniel Gakuba