Friday, July 6, 2012

AZAM INAHITAJI MSAADA WA SIMBA LEO

Wachezaji wa Azam

Na Prince Akbar
HATIMA ya Azam FC kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Urafiki, inatarajiwa kujulikana leo, wakati itakaposhuka dimbani kumenyana na Mafunzo katika mchezo wa mwisho wa kundi A, Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Azam ina pointi mbili tu, baada ya kucheza mechi mbili na kutoa sare zote dhidi ya U23 ya Zanzibar, maarufu kama Karume Boys na Simba SC, wakati Mafunzo haina hata pointi moja.
Simba inaongoza Kundi hilo kwa pointi zake nne na leo itakuwa inamaliza na Karume Boys yenye pointi nne pia.
Azam inatakiwa lazima ishinde na wakati huo huo ikiombea duwa mbaya Karume Boys ifungwe na Simba, vinginevyo hata yosso hao wa Zanzibar wakitoshana nguvu na Mnyama, Wana Lamba Lamba wanaweza kuaga.
Kwa sababu hiyo, mechi za leo zinatarajiwa kuwa tamu na za kusisimua kulingana na kwamba ndizo zitakazoamua timu za kusogea Nusu Fainali.
Jana zilichezwa mechi za Kundi B na Super Falcon iliilaza Jamhuri ya Pemba bao 1-0 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Super Falcon ilipata bao hilo kupitia kwa Mbarouk Marshed dakika ya 44, aliyefumua shuti kali na kujaa nyavuni.
Kwa matokeo hayo, Falcon inaongoza Kundi B, kwa pointi zake tatu, mabao mawili ya kufunga na moja la kufungwa, ikifuiatiwa na Jamhuri yenye pointi tatu pia, mabao matatu ya kufunga na mawili ya kufungwa. Lakini pointi hizo Jamhuri ilivuna mbele ya Yanga, ambayo imeenguliwa.
Ikumbukwe kundi hilo, limebaki na timu tatu tu, nyingine ikiwa ni Zanzibar All Stars baada ya kuondolewa kwa Yanga kwenye michuano hiyo kwa kitendo chao kupeleka timu B, badala ya timu A.
Katika mechi za awali za Kundi A, Simba SC ilitoka sare ya 1-1 na Azam FC juzi.
Simba ilitangulia kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa mshambuliaji wake iliyemsajili kutoka Dong Tam Long An ya Vietnam, Danny Mrwanda, lakini Azam ilisawazisha kupitia kwa George Odhiambo ‘Blackberry’ dakika ya 45.
Abdulhalim Humud alipewa kadi ya pili ya njano na kuwa nyekundu dakika ya 52 na kutolewa nje, hivyo Azam kubaki pungufu ya mchezaji mmoja uwanjani.
Katika mechi yake ya kwanza Jumatatu, Simba SC ilianza vyema baada ya kuifunga Mafunzo mabao 2-1, wakati Azam ililazimishwa sare ya 1-1 na Karume Boys.

kutoka: Bin Zubeiry