Tuesday, July 10, 2012

Hii sasa kali: Benki ya Dunia yawakera wabunge


Mjengoni Dodoma

WABUNGE wamesema Benki ya Dunia ni miongoni mwa vikwazo vya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Masikitiko hayo waliyatoa jana bungeni walipokuwa wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji.
Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbayi (CHADEMA), alisema miradi mingi ya maji inayofadhiliwa na benki hiyo mpaka sasa inasuasua na kubainisha kuwa haridhishwi na kasi ya upatikanaji wa maji licha ya serikali kudai ni sikivu.
Alisema haoni usikivu huo kwa sababu haijawapelekea huduma ya maji na matokeo yake ni wananchi kuishi maisha ya dhiki.
Mbunge wa Bukene, Seleman Zedi (CCM), aliitaka serikali ieleze mradi wa maji ya Ziwa Victoria ulioahidiwa na Rais Jakaya Kikwete, kwamba utafika mkoani Tabora kabla ya mwaka 2015.
Alisema kuwa, mradi huo muhimu unaoonekana kutokamilika kabla ya mwaka huo, unatakiwa kukamilika kama Rais Kikwete alivyoahidi.
 
Makao makuu ya Benki ya Dunia

Kwa mujibu wa Zedi, ahadi ya rais haitakiwi kufanyiwa mzaha na badala yake inatakiwa kutekelezwa kwa haraka ili wananchi wa Tabora waondokane na kero ya maji inayowakabili.
Katika hatua nyingine, alisema tafsiri ya upatikanaji wa maji ya uhakika inayoelezwa na Serikali, haiwezi kukubaliwa kwa kuwa baadhi ya maeneo hayana maji ingawa Serikali inasema maji yanapatikana kwa wingi.
Naye Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agripina Buyogela (NCCR-Mageuzi), alisema haridhishwi na kasi ya miradi ya maji inayofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Alisema pamoja na umuhimu wa maji nchini, miradi hiyo haijakamilika na kwamba umefika wakati sasa Serikali iseme itakamilika lini ili kukabiliana na matatizo ya maji yanayowakabili wananchi.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Selukamba (CCM), alisema kama Vita Kuu ya Tatu ya Dunia itatokea, inaweza kusababishwa na ukosefu wa maji.
Selukamba ambaye alisema haungi mkono bajeti hiyo, alisema ili kuondokana na uhaba wa maji unaowakabili Watanzania, Serikali inatakiwa kuanza kuvuna maji ya mvua na yaliyoko kwenye vyanzo vingine vya maji.
Akizungumzia upatikanaji wa maji Mjini Kigoma, alionyesha mshangao na kusema licha ya mkoa huo kuwa na Ziwa Tanganyika, wananchi wa mji huo hawana maji ya uhakika jambo ambalo alisema haliwezi kuvumiliwa.