Jengo la mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
WAZIRI wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, amesema Serikali inafunga chombo maalumu cha kudhibiti matumizi mabaya ya mtandao ikiwemo wizi unaofanyika.
Prof. Mbarawa alisema hayo jana mjini hapa wakati wa semina ya wabunge kuhusu mtandao iliyoandaliwa na Ofisi ya Bunge kwa ufadhili wa Mpango wa Maendeleo wa umoja wa Mataifa (UNDP).
Alisema mtandao huo utakaowekwa katika ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA), utakamilika Oktoba mwaka huu na kwamba kutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi kuhusiana na uhalifu huo, baada ya kukamilika kufungwa kwa chombo hicho mitandao yote itakayothibitika kukiuka maadili itafungwa.
Waziri alisema pia utaweza kudhibiti matukio ya mzunguko wa fedha unaofanywa na watu wasio waaminifu ambao wanawaibia wateja wa taasisi za fedha na kampuni za simu.
Mbunge wa Kilwa, Abdulkarim Shah (CCM), aliwataka wabunge kujifunza namna ya kutumia mtandao ili wawe wanautumia wakati wakifanya mawasiliano badala ya kutumia vikaratasi.
Shah alisema wabunge wanapaswa kuwa na vifaa vitumiavyo mtandao kama kompyuta ndogo (laptop) na kufanya mawasiliano ili iwe rahisi kwao kuwasiliana.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Kompyuta, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Respickius Casmir, alisema kuwa kuna haja kubwa ya kutoa elimu kwa wananchi ili kuweza kutambua umuhimu wa kutumia mtandao.
Wananchi wanatakiwa kupewa mbinu ya kuhifadhi namba zao za siri ili kuepukana na wizi ambao unaweza kujitokeza kwa njia ya mtandao hususani wizi wa fedha na utapeli.
Habari na Tanzania Daima na Picha kwa hisani ya WamtaaniBlog