mkulima wa kahawa huko Moshi
WANACHAMA wa Chama cha Ushirika cha KNCU (1984) Ltd, wameridhia kuuzwa majengo yake mawili ili kunusuru Kiwanda cha Kukoboa Kahawa Tanzania (TCCCO) kinachodaiwa zaidi ya Sh700 milioni.
Uamuzi wa kuuzwa kwa majengo hayo umetokana na taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa bodi ya chama hicho, Maynard Swai, kwenye mkutano mkuu kwamba akiwanda hicho kinadaiwa Sh757 milioni na uchakavu wa mitambo.
Swai alisema kiwanda hicho kina uchakavu mkubwa wa mitambo, kwani kimejengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita hivyo kusababisha gharama za uendeshaji ikiwamo umeme ambazo hivi sasa wanalipa Sh13 milioni kwa mwezi.
Alisema hivi sasa kiwanda hicho kinadaiwa madeni ya kisheria na uendeshaji, huku akitaja wadai wao kuwa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inayowadai zaidi ya Sh341 milioni.
Wengine ni NSSF zaidi ya Sh126 milioni, Manispaa ya Moshi Sh42 milioni, Astra Insurance Brockers Sh43 milioni, madeni ya wafanyakazi Sh56 milioni, KNCU 1984 Limited Sh70 milioni na madeni ya wagani Sh76 milioni.
Alisema kiwanda hicho kinatarajia mapato yanayotokana na huduma ya kukoboa kahawa, ambayo kutokana na gharama kubwa ya ukoboaji kiwanda kimeshindwa kupata mapato yanayotosheleza kujiendesha.
Swai alisema kahawa inayokobolewa kiwandani hapo imeshuka kutoka tani 65,736 msimu wa mwaka 1980/81 hadi tani 3,787 mwaka 2011/12.
Alisema uwezo wa ukoboaji mashine moja ni tani mbili kwa saa, lakini kutokana na uchakavu umeshuka hadi chini ya tani moja kwa saa.
Habari na gazeti la mwananchi picha kwa hisani ya WamtaaniBlog