Tuesday, July 3, 2012

Vijiji 14 Mufindi kuachana na giza


Shamba la chai Mufindi
ZAIDI ya Sh15.4 bilioni zinatarajiwa kutumika kukamilisha mradi wa umeme wa Mwenga wilayani Mufindi, mkoani hapa.

Meneja mradi huo, Mike Gratwicke, alisema mradi huo mpya utaanza baada Agosti mwaka huu na kwamba, wananchi  wa vijiji 14 wataondoka gizani.

Mradi huo upo Kijiji cha Isipii, Kata ya Ihanu, ulijengwa kwa ushirikiano baina ya Kampuni ya Chai Mufindi (MTC) na Jumuiya ya Ulaya (EU).

Gratwicke alisema wananchi hao wataingia kwenye matumizi ya teknolojia mpya ya ununuzi wa umeme huo utakaokuwa ukiuzwa kama vocha za simu kwa kutumia mawakala mbalimbali watakaojitokeza.
Pia, Serikali na wadau wanataka mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha megawati nne, uzinduliwe Agosti mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete.

Gratwicke alisema awali mradi huo ulikuwa ukamilike Machi mwaka huu, lakini kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwazo usafirishaji mitambo na vifaa vingine vya ujenzi, utazinduliwa Agosti.

Alisema gharama za kuunganishwa itakuwa nusu ya zile zinazotozwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), baada ya EU kuchangia asilimia 49 ya gharama za mradi huo.

“Bado tupo katika mazungumzo na kampuni mbalimbali za simu za mikononi, ili waje wafunge mitambo yao ya simu kwa lengo la kuimarisha mawasiliano vijiji vyote,” alisema.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi