Sunday, July 1, 2012

NSSF kujenga jengo la kibiashara

SHIRIKA la Hifadhi la Jamii (NSSF), linatarajia kuanza ujenzi wa jengo la biashara la ghorofa 33 kwa ajili ya kuongeza vitega uchumi vyake ambavyo vitalisaidia kukuza mapato yake.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, katika maonesho ya Sabasaba katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Ofisa Uwekezaji wa NSSF, Sakina Mbullo, alisema ujenzi huo utaanza wakati wowote kuanzia hivi sasa baada ya kukamilika kwa taratibu zinazotakiwa.
“Jengo hilo linaitwa Mzizima Tower, litakuwa jirani na jengo la Haidary Plaza ambapo liko pale Posta, tumedhamiria kuweka vitega uchumi vingi zaidi ili kupanua wigo wa mapato yetu,” alisema.
Mbullo hakutaka kutaja gharama za ujenzi huo lakini alisisitiza ujenzi utaanza kwa sababu fedha za mradi huo zipo na lengo la NSSF ni kujitanua zaidi.
Aliongeza kwamba ujenzi wa jengo hilo utakuwa na sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza itajengwa jengo lenye urefu wa ghorofa 33 na ya pili itakuwa na ghorofa 20.
Alifafanua kuwa sehemu ya jengo lenye ghorofa 33 litatengwa kwa matumizi ya kibiashara huku lile jingine likitarajiwa kuwa la makazi ya watu.
Mbullo alisema mara kwa mara NSSF imekuwa na kawaida ya kujenga majengo ya kisasa na hilo litakalojengwa litaendana na viwango vya kimataifa ambavyo tayari michoro yake inafanyiwa kazi.
Alibainisha kuwa awali jengo hilo lilipangwa liwe la ghorofa 45 lakini baada ya tathmini ya gharama kufanyika ikaamriwa lijengwe la ghorofa 33 likitenganishwa na lile la makazi.

Source: Tanzania Daima Jumapili