Askari wa JWTZ
Ndege ya kivita ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) imeanguka na kusababisha kifo cha mwanajeshi mmoja na kujeruhiwa mmoja wakati wakiwa katika mafunzo ya kurusha ndege.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, akizungumza na NIPASHE alithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana majira ya saa 4:28 asubuhi makao makuu ya kambi ya Jeshi la Anga (Air Wing) eneo la Ukonga, jijini Dar es Salaam.
Kanali Mgawe alimtaja mwanajeshi aliyepoteza maisha kuwa ni Kapteni Gatius Magushi ambaye alikuwa na mwenzake wakifanya mazoezi ya kijeshi ya namna ya kurusha ndege.
Alisema marehemu Mgushi wakati wa mafunzo hayo alikuwa na mwenzake kapteni Kwidike ambaye namejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Kijeshi ya Lugalo.
Kanali Mgawe alisema wanajeshi hao wakiwa katika mafunzo hayo, baada ya kuwasha ndege, iliruka mita 100 kutoka usawa wa bahari na baada ya muda mfupi ilipata hitilafu na kuanguka.
“Kwa kawaida ndege ikisharuka inapokuwa angani hutakiwa viti vilivyomo katika ndege hiyo kufyatuka tayari kwa marubani hao kuruka kwa kutumia maparashuti,” alisema Kanali Mgawe.
Aliongeza kuwa baada ya viti vya ndege kufyatuka, rubani mmoja hutakiwa huruka kwenda upande wa kushoto na mwingi upande wa kulia.
Alisema kilichotokea ni kwamba viti vya marubani hao vilifunguka pamoja na maparachuti yao yalifunguka, lakini kwa bahati mbaya aliyedondokea upande wa kulia alifikia juu ya paa na alifariki hapo hapo na aliyerukia upande wa kushoto aliangukia kwenye lami na kujeruhiwa .
Kanali Mgawe alisema hata hivyo, ndege hiyo haijaharibika sana isipokuwa kifaa kinachotumika kupimia mwendo kasi pamoja na bawa moja vimeharibika.
CHANZO:
NIPASHE