Mheshimiwa George Mkuchika.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika ni miongoni mwa majina ya wanachama watatu walioteuliwa na uongozi mpya wa Yanga kuwa wajumbe wa Bodi ya Udhamini ya klabu hiyo ya ‘Jangwani’.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Yanga, Selestine Mwesigwa, aliwataja wajumbe wengine wapya wa bodi yao ya udhamini kuwa ni Seif Ahmed 'Magari' na Balozi Army Mpungwe.
Awali, viongozi wapya wa klabu hiyo waliochaguliwa Julai 15 katika uchaguzi wao mdogo waliapishwa na mke wa Rais wa awamu ya kwanza wa Zanzibar, Mama Karume. Walioapishwa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo, Aaron Nyanda, Mussa Katabaro na George Manyama.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa, alisema vilevile kuwa uongozi mpya wa klabu hiyo umezifuta kamati zao zote za uongozi klabuni hapo.
Mwesigwa alisema kuwa uongozi pia umekubaliana kuifanyia marekebisho katiba ya klabu hiyo ili iendane na wakati uliopo.
Alisema kuwa uongozi huo umekubaliana pia kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima kwa kufanya shughuli mbalimbali za utendaji kwa kufuata maelekezo yaliyoko kwenye katiba yao.
Hata hivyo, jana kabla ya viongozi hao hawajaapishwa, wanachama mbalimbali waliokuwepo klabuni hapo walitaka wajumbe Sarah Ramadhan, Mohamed Bhinda na Salum Rupia wasiingie kwenye jengo hilo, wakiwatuhumu kwamba si waaminifu.
Wanachama hao walisema kwamba wakati wa harakati za kuutaka uongozi wa Mwenyekiti, Lloyd Nchunga ujiuzulu, wajumbe hao walionekana kutokuwa na msimamo.
Wanachama hao wameupa uongozi wiki moja kuhakikisha wanawaondoa wanachama hao kwenye madaraka ili wasiwachanganye kwa sababu wanaamini hawaitakii mema klabu yao.
Endapo viongozi hao wataondolewa, itabidi Yanga ifanye tena uchaguzi mdogo au isiburi hadi mwaka 2014 itakapofanya uchaguzi mkuu.
CHANZO:
NIPASHE