Thursday, August 2, 2012

Polisi kuwa linda Walimu huko Moshi

http://www.policeforce.go.tz/images/stories/fruit/s3.gif 
Polisi akiwa kwenye farasi..

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limesema litawalinda walimu ambao wanapenda kuendelea na kazi ili wasibugudhiwe na wale ambao hawataki kuendelea na kazi kwa kuwa wako kwenye mgomo.

Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Robert Boaz, imesema kuwa Jehi hilo litachukua hatua za kisheria dhidi ya watakaobainika kuvunja sheri za nchi ikiwemo kutumia wanafunzi kuandamana ili kudai haki zao.

“Jeshi la Polisi lina wajibu wa kusimamia sheria, kulinda raia na mali zao, tunawajulisha walimu wote wanaotaka kufundisha wafanye kazi zao
na endapo kuna mtu yeyote anayewatisha, kuwaingilia au kuharibu mali watoe taarifa mara moja,” alisema.
  

Katika hatua nyingine, zaidi ya walimu 607 wa shule za msingi na sekondari mkoani humo, walishiriki kwenye mgomo ulioanza juzi.

Taarifa kutoka idara ya elimu ya mkoa imeeleza kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na maafisa elimu wa wilaya za mkoa huo, imeonyesha kuwa mgomo ulikuwa mkubwa juzi, lakini unaendelea
kupungua.

Katika wilaya ya Rombo kati ya walimu 156 wa shule za msingi 74 walisaini na kuondoka na 12 hawakwenda shule kabisa, huku shule za
sekondari 41 zilizopo walimu 50 walisaini na kuondoka.

Wilaya ya Hai, shule za sekondari za Lemira, Harambee, Uduro, Lyasikika walimu walikuwa kwenye mgomo na shule hizo kubakiwa na walimu wakuu pekee na kwamba jumla ya walimu 182 walikuwa kwenye mgomo.

Wilaya ya Moshi Vijijini shule za msingi Mabogini, Kibosho, Marangu na Kahe walimu waliripoti na kisha kuondoka huku shule ya Sekondari ya
Mangi Marealle ikibakiwa na mkuu wa shule pekee na kwamba kwa wilaya hiyo asilimia 50 walikuwa kazini ila asilimia 10 ndiowalisaini na kuondoka.

Katika wilaya ya Mwanga, Shule ya Sekondari ya Kigonigoni alibaki mkuu wa shule pekee, huku shule za sekondari za Kifaru, Kwangu, Kilomeni, Kileo na Asha Rose Migiro mahudhurio ya walimu yalikuwa ni asilimia 50.

Wilaya ya Siha, walimu 129 waliripoti na hawakufanyakazi, 12 hawakuripoti kabisa na 34 ndio waliokuwa wanafanyakazi huku walimu 454 wa shule za msingi wakigoma.

Katika wilaya ya Same, shule za sekondari za Hedaru na Makanya hakukuwa na walimu kabisa.

Manispaa ya Moshi, walimu 96 wa shule za sekondari wamegoma huku 115 wakiendelea na shughuli zao wakati shule za msingi walimu 147 walikuwa kwenye mgomo na 186 walikuwa kazini.