Mr Hamis Mgeja wa kwanza Kushoto.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja, amempongeza Naibu waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele kwa hatua alizoanza kuchukua kwa ajili ya kutatua kero za wachimbaji wadogo wa madini nchini.
Mgeja, alitoa pongezi hizo juzi alipokuwa akitoa salamu zake kwa wakazi wa mji wa Kahama mkoani Shinyanga, katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Masele.
Mbali ya kumpongeza Masele, alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya kwa jinsi ambavyo amekuwa mstari wa mbele kushughulikia matatizo ya wananchi.
Alisema katika kipindi kifupi, tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo, ameweza kutatua baadhi ya kero za wachimbaji wadogo wa madini katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Shinyanga na Kigoma.
“Tunakupongeza sana kwa juhudi unazozionesha katika kuwasaidia Watanzania, hasa ndugu zetu wachimbaji wadogo wa madini mbalimbali hapa nchini, kule Arusha ulipewa jina la Mussa, leo sisi hapa tunakupa jina la Muarobaini wa kupambana na matatizo ya wachimbaji wadogo.”
Kwa upande wake, Waziri Masele alisema wizara yake hivi sasa, inafanya kila jitihada, ili kuhakikisha inapitia upya mikataba yote ya madini nchini, ili kuwezesha wananchi waweze kunufaika.
Alisema wizara yake, tayari imeanza kuchukua hatua za kuhakikisha Tanzania inakwenda kasi katika suala zima la maendeleo kwa kupunguza kiwango cha umasikini kwa wananchi wake.