WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo amewataka wavuvi kusajili chama chao cha Muungano wa Wavuvi Tanzania (TAFU) kuwa Chama Kikuu cha Ushirika ili serikali iwakabidhi jukumu la kusimamia upangaji wa bei ya samaki.
Alisema iwapo wavuvi hao watakuwa katika chama cha ushirika serikali itawaruhusu kuuza samaki kwenye viwanda vya samaki kwa bei ambayo itapangwa kama elekezi, na kwamba itaondoa matatizo ya sasa ya mvutano wa bei za samaki baina ya wavuvi na wenye viwanda.
Awali wakizungumza kwa nyakati tofauti, mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo, na Maji, wavuvi hao walidai kuwa wamekuwa wakiuza samaki wao aina ya Sangara viwandani kwa Bei ya Sh 3000 hadi Sh 3200 huku baadhi ya mawakala wa viwanda hivyo ambao wamekuwa wakipewa fedha na viwanda wakinunua samaki hao mialoni kwa Bei Sh. 4,000 hadi Sh. 5,000.
Akieleza malalamiko yao kwa niaba ya wavuvi, Mwenyekiti wa TAFU Juma Chamoto, alisema wavuvi wamekuwa wakipewa bei ndogo ya samaki na wamiliki wa viwanda vya samaki kwa kisingizio cha kushuka kwa bei ya samaki katika soko la dunia wakati samaki ambao wamekuwa wakiwauzia wamekuwa wakitoa mazao mengine kama mafuta, mabondo, ngozi, mapanki, kifua, pamoja na kichwa ambavyo vyote wamekuwa wakiviuza pia.
“Samaki akishuka bei kwenye soko la dunia wanashusha bei kwetu, lakini wakinunua samaki wetu wanachukua na mazao mengine lakini hivi vyote licha ya kuviuza hawataki kutuongezea bei ya samaki wakijua kuwa hivi navyo vinawapatia faida,” alieleza Chamoto.
Alimweleza waziri na wabunge kuwa wanachokitaka ni serikali kupanga bei elekezi ya samaki ambayo itawashirikisha wavuvi ama wawakilishi wao na kama hata bei ikishuka katika soko la dunia basi bei itakayouzwa samaki hao izingatie faida ya mazao mengine ya samaki.
“Bei ya Panki pekee kwa kilo moja ni sh. 400, Bondo ni sh. 150,000 kwa kilo moja, mafuta ya sangara ni sh. 300 kwa kilo na kifua ni sh. 600 kwa kilo moja, hivi vyote vinapatikana kwenye samaki ambao tunawauzia, lakini wanapotushushia bei hawataki kuviona hivyo na badala yake wananunua kilo moja ya samaki kwa sh. 3200,” alieleza Petro Mtatira mmoja wa wavuvi hao.
Kwa upande wake Juvenalis Matagiri alisema iwapo wamiliki wa viwanda hawataki kutoa bei yenye maslahi kwao serikali iruhusu wao kuuza samaki wao nchi jirani za Kenya na Uganda ambako wanatoa bei ya juu zaidi kuliko viwanda vya ndani, ombi ambalo waziri alikubaliana na wavuvi kutembela nchi hizo kujifunza zaidi.
Hata hivyo kutokana na mjadala wa muda mrefu walikubaliana kuanzishwa kwa Chama cha Ushirika ndani ya wiki moja ili kuharakisha kuwa na chombo cha kuwasimamia wavuvi hao.
Kutokana na makubaliano hayo Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Neema Mgaya Ahmed alimtaka waziri kuhakikisha chama cha ushirika cha wavuvi hao kinasajiliwa na kwamba kisiposajiliwa katika kipindi cha siku saba, basi watagomea bajeti ya wizara yake.
Kikao hicho kilitarajiwa kuendelea kwa waziri na kamati hiyo kukutana na wamiliki wa viwanda ili kusikiliza upande wao na kisha kutoka na azimio la pamoja.