Monday, July 23, 2012

BOA Tanzania yaanzisha mikopo ya Bima


BOA Bank


Benki ya Afrika Tanzania imezindua huduma ya mkopo wa bima kwa lengo la kuboresha huduma kwa wateja wake na kuongeza ubunifu.

Akizindua huduma ya mkopo huo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Ammish Owusu-Amoah, alisema huduma hiyo ya mkopo wa bima itawasaidia wateja kukopeshwa fedha kwa ajili ya kulipia bima za vitu mbalimbali ambazo mara nyingi huhitaji fedha nyingi kwa wakati mmoja.

“Huduma hii itawasaidia wateja kuwa na nafasi ya kutumia fedha zao kwa maendeleo huku wakiendelea kulipa mkopo wa bima taratibu,” alisema.

Alifafanua kuwa mkopo huo utakuwa kwa watu binafsi, wafanyabiashara ndogo na kati pamoja na wateja wakubwa.

Alisema ni muhimu kwa watu kuweka bima ili kujihadhari na hatari zisizofahamika ambazo zinaweza kutokea wakati wowote.

Alifafanua kwamba huduma hiyo itasaidia wateja kupata mkopo ndani ya saa 24 na kuwezesha kulipa taratibu ndani ya miezi 10.  

Alitaja maeneo yanayolengwa kwa sasa kama bima ya maisha, bima ya magari, bima ya mali na bima ya biashara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha wafanyabiashara wadogo na wa kati katika benki hiyo, Cyprian Massawe, alisema hiyo ni nafasi ya pekee kwa wafanyabiashara nchini katika kuendeleza biashara zao.

Alisema sasa bima imekuwa ni sehemu muhimu ya maisha ya kila siku sehemu mbalimbali duniani.

Alitoa mfano wa mafuriko yaliyotokea jijini Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchini  hivi karibuni na kwamba yalisababisha hasara kubwa kwa kwa mali na maisha ya watu.