Monday, May 28, 2012

Saccos Kilombero yakopesha wanachama Sh900 milioni

Ifakara
5000 tz shillings front.jpg10000 tz shillings back.jpgCHAMA cha Kuweka na Kukopa cha Wafanyakazi wa Halmashauri ya Kilombero (KDWS), mkoani Morogoro kimewakopesha wanachama wake zaidi ya Sh965.3 milioni ili kupambana na umasikini.
Mwenyekiti wa   Saccos hiyo, Hawa Ngaoneka alisema hayo mwishoni mwa wiki alipozungumza na waandishi wa habari waliotembelea Saccos yake ili kujionea mafanikio ya wanachama katika kupambana na umasikini.
Alisema Saccos yake  yenye wanachama 700  kwa mwaka jana pekee iliweza kukopesha zaidi ya Sh965.3 milioni  kwa wanachama wake 773 wakiwamo watatu waliokopa matrekta mawili aina ya Powertiller na moja trekta kubwa.
Alisema wanachama 464 kati ya hao walikopa mikopo ya dharura, wakati  wengine 285 walikopa mikopo ya kawaida, wengine 21 walikopa ya biashara huku watatu wakichukua matekta.
Baadhi ya miradi ya maendeleo ya wanachama wa Saccos hiyo iliyotembelewa na waandishi wa habari ni maduka ya dawa na ujenzi, mabasi na mashine za kukoboa mpunga na mashamba.
Ngaoneka alisema fedha za kuwakopesha wanachama zilitokana na michango yao pamoja na mikopo wa Sh 600 milioni kutoka Mfuko wa Pensheni wa LAPF  uliotolewa kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2008 na 2011.
Ngoneka alisema Saccos yake  kwa sasa inajiandaa kwa mwaka ujao ili kukopa tena LAPF Sh600 milioni  zingine kwa mkupuo zitakazowanufaisha zaidi  wanachama wa Saccos  hiyo.
Akizungumzia sababu za Saccos hiyo
kupata mikopo hiyo, Ofisa Masoko wa LAPF, Rehema Mkamba alisema ilipata fedha hizo baada ya kutimiza vigezo na kwamba mpango huo uko wazi kwa Saccos  za wanachama katika halmashauri zote nchini.
Mkamba alisema LAPF inazikopesha Saccos za wanachama wa mfukjo ili waweze kupunguza umasikini na kwamba lengo ni kujenga maisha yao kabla ya kustaafu.