BAADHI ya maduka ya kuuza dawa muhimu mjini Kigoma yamedaiwa kukiuka kanuni na utaratibu wa utendaji wake kwa kuuza dawa za kutibu ugonjwa wa kifua kikuu (TB) kiholela, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Uchunguzi uliofanywa na Asasi ya Mapambano ya Kifua Kikuu na Ukimwi Tanzania (Mkuta), mkoani Kigoma umebaini kuwepo kwa dawa hizo kwenye maduka ya dawa baridi ya jumla na rejareja, hivyo kukiuka sheria inayoelekeza dawa hizo zitolewe bure katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizoteuliwa rasmi na mamlaka husika.
Mratibu wa Asasi ya MKUTA Mkoa wa Kigoma, Maulidi Ntahondi alibainisha ukiukwaji huo wa sheria akitaja maeoneo husika kuwa ni Kigoma mjini, Bangwe, Gungu na Mwanga na kwamba maelekezo yanayotolewa na wahudumu wa maduka hayo kuhusu utumiaji dawa hizo yanatofautiana.
Aliongeza kuwa dawa hizo huuzwa kwa Sh10,000 kwa boksi moja ambapo pia dozi moja ya vidonge ishirini huuzwa kwa Sh4000.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dk Yakayashi Macrice alisema kuuza dawa za kutibu TB kwenye maduka hayo binafsi ni kosa kisheria na kwamba wahusika wanastahili kukamatwa na kufikishwa mahakamani.
Alisema kuwa dawa hizo zinatolewa na Bohari Kuu ya Dawa ya Serikali na zinapaswa kutolewa bure kwa wagonjwa wa TB na kwamba ni lazima zitolewe katika vituo vya afya, hospitali au kwenye zahanati maalumu zilizoteuliwa kulingana na jiografia ya wilaya husika zikiwa na wataalamu wa afya.
Alimuagiza Mfamasia Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuhakikisha kuwa wote wanaouza dawa hizo kwenye maduka binasfi wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.
Baadhi ya watumishi wa maduka binafsi ya dawa yanayouza dawa hizo bila kufafanua walieleza kuwa dawa hizo za TB huuzwa kwa kuwa zina matumizi tofauti na kutibu ugonjwa huo.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi