 
 
Sheikh Hamis Mattaka(kushoto)  
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Dar es Salaam.
Taasisi
 ya masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imeunga mkono kauli 
iliyotolewa hivi karibuni na Sheikh mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban
  Simba ya kuwataka waislamu na watanzania  kote nchini kushiriki 
kikamilifu katika Sensa ya watu na Makazi itakayofanyika  Agosti 26 
mwaka huu.
Akizungumza
 na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya mwenyekiti
 wa jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania Sheikh Hamis 
Mattaka amesema hatua hiyo inafuatia kuwepo kwa baadhi ya makundi 
yanayowahamasisha waumini wa dini ya kiislamu na wananchi kutoshirika 
zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Amesema
  wao kama jopo la wanazuoni hawaoni tatizo la zoezi hilo kutokana na 
umuhimu wake kwa taifa na kuongeza kuwa  Sensa ya watu na makazi ipo kwa
 mujibu wa sheria za nchi na imepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano
 wa Tanzania.
Jopo
 hilo  limeiomba serikali kuweka sheria itakayozuia utoaji wa takwimu 
zinazohusu dini za watanzania zinazotolewa na vyanzo mbalimbali ndani na
 nje ya nchi kwa kuwa kipengele hicho si sehemu ya sensa nchini.
“Tunajua
 kuwa serikali ilikua na nia njema kukiondoa kipengele cha dini katika 
Sensa hapana budi nia njema hiyo ya serikali ilindwe kwa kuweka sheria 
itakayozuia kutoa takwimu zinazohusu dini za watanzania” amesema Sheikh 
Mattaka.
Amefafanua
 kuwa Sensa ya awali ya mwaka 1957 kipengele cha dini kilihusishwa na 
baadaye kuondolewa katika Sensa zilizofuata kwenye madodoso ya 
kukusanyia takwimu za kaya.
“Sisi
 kama jopo kila siku tunasema ili twende salama kama wananchi wa nchi 
hii ni wajibu wetu  kuheshimu na kufuata sheria kwa maana ya kutii 
sheria bila shuruti, kwa hiyo tunasema Sensa ya watu na makazi ni jambo 
la kisheria si jambo la mitaani, hatuwezi kulumbana na kujadili jambo 
ambalo liko wazi kisheria na limepitishwa na wabunge tuliowachagua sisi 
wenyewe”
Amefafanua
 kuwa zoezi la Sensa ya watu na makazi litaiwezesha serikali kupanga 
mipango ya maendeleo kwa kuwa na takwimu sahihi za watu na makazi, hali 
ya kipato cha kaya, vizazi na vifo na pia kuiwezesha serikali kwapatia 
huduma bora wananchi wake.
Katika
 hatua nyingine jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania 
imewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ukusanyaji wa
 maoni ya katiba.
Aidha
 jopo hilo limewataka watanzania wote kwa ujumla kuitumia fursa hiyo 
muhimu kutoa maoni ambayo yataiwezesha nchi kupata katiba itakayokidhi 
matakwa ya wananchi.
“
 Sisi kama jopo la wanazuoni wa kiislamu tunawataka waislamu na 
watanzania wote kwa ujumla kuitumia fursa hii muhimu kwa kutoa maoni yao
 ili hatimaye nchi yetu ipate katiba itakayokidhi matakwa ya wananchi 
kwa miaka mingi ijayo” amesema Sheikh Mattaka.
Chanzo: Mjengwa Blog 
 
 
 
 Tanzanian Shilling Exchange Rate
    Tanzanian Shilling Exchange Rate