Monday, July 23, 2012

SSRA: Mafao ni miaka 55 kwa Wanachama wa NSSF, PPF


 
Mkurugenzi Mtendaji wa SSRA Bi Irene Isaka (kushoto)

Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), imesema kuanzia sasa mwanachama wa mfuko wowote hataruhusiwa kuchukua mafao yake kutokana na sababu yoyote mpaka hapo atakapofikisha miaka 55.

Hata hivyo, licha ya kuzuia fao la kujitoa na kutoruhusiwa kuchukua mafao yao, mwanachama wakiwamo wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma NSSF) atapata fursa ya kupata mikopo ya nyumba kwa kutumia dhamana ya michango yake kama ilivyoelezwa kwenye sheria ya SSRA.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka, mabadiliko hayo yametokana na sheria za mamlaka hiyo kufanyiwa marekebisho na kupitishwa na Bunge Aprili 13, mwaka huu na kwamba imeshasainiwa na Rais Jakaya Kikwete  na imeanza kutumika rasmi.

Kwa mujibu wa marekebisho hayo fao la kujitoa yamefutwa na kuanzia sasa hayatakuwepo.
“Mafao hayo yalikuwa yanatolewa pale mwanachama alipokuwa anaacha kazi lakini kuanzia sasa mwanachama wa mfuko atapata mafao yake pale atakapofikisha umri wa kustaafu kwa hiari (55) au kwa lazima (60) au pale anapopata ulemavu wa kudumu” ilisema  taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na kufafanua kuwa:

“Marekebisho hayo kuhusu kuzuia mafao ya kujitoa yamefanyika ili kutimiza lengo na madhumuni ya hifadhi ya jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa mwanachama anapostaafu anapata mafao bora yatakayomwezesha kumudu maisha ya uzeeni.

 Taarifa ya Mkurugenzi huyo iliendelea kusema  kuwa mafao ya kujitoa yanapunguza na kuondoa  kinga ya mfanyakazi pale anapoumia kazini au anapofika uzeeni.

Hata hivyo, ilisema pamoja na kuzuia fao la kujitoa, mafao mengine ambayo ni muhimu kwa sekta ya madini yataendelea kutolewa kama kawaida ikiwemo kuumia kazini pamoja na fao la ulemavu.

Ilisema wanachama wanatakiwa kuwa watulivu kuhusiana na mabadiliko hayo na kwamba maslahi  yao yatalindwa na hakuna atakayepunjwa kutokana na utaratibu huo.