Monday, July 23, 2012

Ratiba mpya Ligi Kuu Bara mwezi ujayo




Shirikisho la Soka Nchini (TFF) limesema kuwa litatoa ratiba kamili ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu ujao wa mwaka 2012/ 2013 Agosti Mosi mwaka huu.

Ligi hiyo itakayoshirikisha timu 14 kutoka mikoa mbalimbali nchini, itaanza Septemba Mosi mwaka huu.

Kabla ya ligi hiyo kuanza, kutakuwa na mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo wa Ngao ya Jamii utakaofanyika Agosti 25 kati ya mabingwa wa ligi hiyo, Simba dhidi ya mshindi wa pili, Azam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba, alisema ratiba hiyo iko katika hatua za mwisho za kuihakiki na imezingatia majukumu ya timu ya taifa (Taifa Stars) na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Kawemba alisema pia ratiba hiyo itazingatia jiografia ya nchi yetu na TFF inazitakia klabu zote zitakazoshiriki ligi hiyo maandalizi safi ili ligi iwe na ushindani.

Timu zitakazoshiriki ligi hiyo inayotoa wawakilishi wa Bara katika mashindano ya kimataifa ni pamoja na mabingwa Simba, Azam, Yanga, Coastal Union, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, JKT Ruvu, JKT Oljoro, Mgambo JKT, Polisi Morogoro, Toto African, Prisons, African Lyon na Ruvu Shooting.

Simba ndio wawakilishi wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika mwakani wakati Azam kwa mara ya kwanza itapeperusha bendera ya nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.

Hata hivyo, mdhamini mkuu wa ligi bado hajatangazwa kutokana na TFF bado kuwa kwenye mazungumzo na kampuni ya huduma za simu ya Vodacom.