Tuesday, August 7, 2012

Wawili wafa, 24 hoi ajali magari Arusha

Watu wawili wamefariki dunia na wengine 24 kujeruhiwa baada ya basi dogo walilokuwa wakisafiria kutoka Moshi kwenda Arusha mjini kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebeba mchanga aina ya Fuso.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo maeneo ya Tengeru wilayani Arumeru jana mchana.

Alisema waliofariki dunia ni dereva na utingo wa basi dogo ambao majina yao hayakupatikana mara moja.

Kamanda Sabas alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi dogo kujaribu kulipita gari lingine na wakati akifanya hivyo, lilitokea lori hilo na kugongana.

Alisema wakati ajali hiyo ikitokea lori hilo liliparamia tena gari dogo aina ya Toyota Chaser.

Alisema majerusi sita wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na 12 wamelazwa kwenye zahanati ya Tengeru na wengine wanne walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka.


SOURCE: NIPASHE