VIONGOZIi wa ngazi mbalimbali wameombwa kutokuwatia katika vishawishi makarani wa sensa ili wajue siri za watu mbalimbali katika maeneo yao.
Hayo yalisemwa na Mkufunzi wa Sensa Mkoa wa Geita, Dietrick Kaijanangoma, wakati akizungumza na Tanzania Daima mjini hapa.
Alisema kuwa kila taarifa za zoezi hilo la sensa linalotegemea kufanyika wiki ijayo zitakazochukuliwa kuwa ni siri kwani makarani watakaofanya kazi hiyo wamekula viapo.
Aliwataka makarani kufahamu kwamba kiongozi yeyote hana mamlaka ya kumlazimisha amwambie jambo lolote alilokusanya katika zoezi la kuhesabu watu hivyo amewataka kufanya kazi zao bila kubughudhiwa katika hilo.
Nasema hivi mwenye mamlaka ya kutangaza idadi ya watu ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ambapo mwezi wa 12 mwaka huu ndiyo atatoa taarifa na si mtu mwingine,” alisema Kaijanangoma.
Alitoa rai kwa wananchi kuwaona makarani kama watu wa kawaida hivyo kuwa wepesi kutoa taarifa zao za kaya ambazo zitasaidia kujua mahitaji ya watu wa rika mbalimbali na hakuna mtu mwingine atakayejua taarifa zao.
Aliwataka wananchi kutunza kumbukumbu za watu watakaolala usiku wa kuamkia Agosti 26 kwani hata karani kama hajapita tarehe hizo akapita siku tatu zijazo hawana budi kutoa taarifa.