Sunday, June 24, 2012

Watanzania wengi wanatembea wamelewa

WAKATI Serikali ikilalamika kuwa uwezo wa wananchi wake wengi kufanya kazi unapungua, imebainika kuwa idadi kubwa ya watu wanafanya kazi na kutembea, wakiwa wamelewa.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili, uliofanywa kwa muda mrefu, umebaini kuwa hivi sasa watu wengi wanakunywa pombe kali zilizofungwa kwenye mifuko ya nailoni maarufu kama viroba, zinauzwa mitaani kama njugu.

Pombe hizo ambazo hivi sasa zinauzwa na wauza karanga, sigara na magazeti mitaani katika maeneo ya miji mikubwa nchini, watumiaji wanaanza kununua kuanzia asubuhi hadi usiku.
Ukiangalia vifurushi vya bidhaa za wafanyabiashara, hasa machinga,  hutakosa kuona viroba kadhaa vya pombe hizo wakiwa wameshikilia mikononi kutafuta wateja.
Awali, vileo vilikuwa vikiuzwa kwenye maeneo maalumu kama vile baa, klabu za usiku, au kumbi za sherehe, lakini sasa hali hiyo imebadilika na sasa watu wengi wanaonekana mitaani kuanzia asubuhi wakiwa wamekunywa na wamelewa. 

Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa, mbali ya wauza karanga na wafanyabiashara ndogondogo kutembeza mitaani pombe hizo kusaka wateja, hata wale wanaouza bidhaa zao kwenye meza sasa viroba ni bidhaa yao mpya.

Hivi sasa ukitembea katika maeneo ya mijini hususan jijini Dar es Salaam huwezi kukosa kuona maganda mengi ya viroba vilivyotumika yakiwa yamezagaa mitaani.Imebainika kuwa wafanyabiashara wengi ndogondogo wamehamasika kuuza viroba kutokana na kuongezeka kwa mahitaji yake.

Mwandishi wa habari hizi ambaye alitembelea maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ikiwamo Stendi Kuu ya Mabasi ya Ubungo, vituo vikubwa vya daladala vya Ubungo, Kinondoni, Mwenge, Mbagala, na maeneo ya masoko, alishuhudia wauza maji, juisi, pipi na sigara wakiwa wamechanganya na viroba wakitafuta wateja, huku baadhi ya watu, wakiendelea kutumia vileo hivyo.

Wauzaji
Baadhi ya wauzaji wa pombe hizo wanasema kuwa soko la pombe kali linaongezeka kwa sababu ya ongezeko la watumiaji.
Amina Ramadhani, mfanyabiashara wa vocha za simu, juisi na maji, maeneo ya  Tabata Relini anasema, viroba vina wateja wengi, ndiyo maana ameamua kuviweka miongoni mwa bidhaa zake.

“Nilianza kuuza viroba baada ya kuona watu wengi wanaviulizia. Kwa sasa ninauza aina zote za viroba,” anasema.  Amina anasema, awali alidhani wafanyabiashara wa bidhaa ndogondogo kama pipi, biskuti, maji ya kunywa na juisi hawawezi kuuza viroba, lakini alipoona wenzake wanauza kwa wingi na vinapata wateja, aliamua kujitosa na kutafuta mtaji wa pombe hizo.

Mfanyabiashara ndogondogo katika maeneo ya Stendi ya Ubungo jijini Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina moja la Issa alipoulizwa kama anauza viroba alijibu: “Nilikuwa navyo boksi zima,  lakini vimeisha saa 4:00 asubuhi,” 

Anasema wateja wake wakubwa ni wasafiri wanaokwenda mikoani, madereva wa mabasi, pamoja na wafanyakazi katika ofisi za mabasi zilizopo kituoni hapo.

“Kwa nyakati za asubuhi, nafanya biashara ya viroba ndani ya basi. Ndani ya basi ninapata wateja wengi tu wanaosafiri, hata madereva na makondakta wa mabasi nao hununua,” anasema Issa.
Mfanyabiashara mwingine, Frank Musa, anasema kwa machinga wa Ubungo, kutokuuza viroba ni sawa na kuuza nyama bila kisu.

“Viroba vinauzika sana asikuambie mtu, tunapata hata wateja wanawake siku hizi,” anasema Mussa.
Biashara ya viroba haifanyiki na wamachinga tu, bali sasa inafanywa pia na  wafanyabiashara wa magenge ya bidhaa za vyakula mitaani.

Thadey Mtei, mfanyabiashara wa genge maeneo ya Tabata Mawenzi anasema viroba ambavyo wateja wake wakubwa ni wanaume na wanawake huanza kuviuza kuanzia asubuhi.

“Mara nyingi hadi saa 4:00 asubuhi huwa tayari nimeshauza viroba vinne hadi sita, bado jioni,” anasema Mtei. Mtei anasema kwa siku huuza viroba zaidi ya 20.

Halikadhalika Mtei hasiti kutaja majina ya wateja wake wakubwa ambao wengi ni wanawake na anafafanua kuwa, wengi huanza kunywa tangu asubuhi.   Wafanyakazi Utumiaji wa viroba sio tu kwa watu wasio na ajira bali hata baadhi ya wafanyakazi katika maofisi mbalimbali.
Uchunguzi unaonyesha kuwa wafanyakazi katika maofisi hayo yakiwamo ya Serikali wamekuwa wakiingia kazini wakiwa wamelewa huku wengine wakiwa na viroba mifukoni.

“Nimeshawahi kumshuhudia trafiki akiwa amelewa nilimgundua baada ya kumsimamisha dereva wa daladala tulilopanda na kumsikia akitoa harufu ya pombe,” anasema Editha Majura
Watumiaji wanasemaje?   Yohana Ibrahim Mkazi wa Tabata, anasema yeye hunywa viroba  kwa ajili ya kupunguza mawazo.

“Mimi sinywi pombe asubuhi, naanza usiku. Sababu inayonifanya ninywe pombe ya viroba ni kupunguza mawazo, ili usiku nilale kwa amani,” anasema Ibrahim.

Anasema hutumia zaidi viroba badala ya bia kwa sababu za kiuchumi. “Viroba ni bei rahisi. Nikinywa vitatu inanigharimu Sh 1,800 au Sh1500, na ninalewa. Lakini kwa hela hiyo, nikinywa bia, labda ni bia moja tu na bado hainileweshi,” anasema Ibrahimu ambaye ni mfanyabiashara anasema, bei ya viroba huanzia Sh500 hadi 600, kulingana na aina ya bidhaa yenyewe.

Wataalamu Mkuu wa Idara ya Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo anasema ongezeko la watumiaji wa pombe kali linatokana na mambo makuu mawili; msongo wa mawazo na ukosefu wa ajira.

“Wengi wanaamini kuwa wakinywa pombe watapunguza mawazo na kwa wale wasio na kazi ni kwa sababu tu ya ukosefu wa kitu cha kujishughulisha,” anasema.

Anasema ongezeko hili linaletwa pia na matatizo ya kijamii na binafsi.  Anatoa mfano, watu wengi wanaoachishwa kazi, talaka, maradhi na mifarakano ya kifamilia hujikuta wakiikimbilia pombe kama suluhisho la matatizo yao.

Dk Kitila anaongeza kuwa wengi wanakimbilia pombe kama mkombozi wao kwa sababu Tanzania haina huduma bora za kisaikolojia.

“Wanaumizwa na msongo wa mawazo na wasiwasi na wanakosa huduma za ushauri, ndiyo maana wanaamua kujitibu wenyewe,” anasema Kitila.  Wakati huo huo, utafiti uliofanywa na Shirika la Afya na Utafiti Afrika (AMREF), umeonyesha kuwa, idadi ya Watanzania wasiokuwa na ajira ilifikia asilimia 10.7 mwaka jana.   Utafiti Utafiti uliofanywa mwaka 2003, na Joyce Kinabo kuhusu utandawazi, mfumo wa chakula na madhara yake katika usalama wa chakula, tafiti zilionyesha kuwa, uzalishaji wa pombe nchini ulianza kuongezeka kuanzia miaka ya 1990.

Katika utafiti huo Kinabo anasema, aina ya unywaji inabadilika siku hadi siku. Hapo zamani pombe hazikutengenezwa kwa ajili ya kuuzwa. Pombe zilitengenezwa kwa ajili tu ya sherehe au tukio maalumu.

Unywaji wa pombe ulipoanza kufanywa biashara watu wamekuwa wakinywa bila malengo.
Hiyo imesababisha maeneo mengi ya kuuza pombe kufunguliwa hata pale yalipo makazi ya watu.
Mkurugenzi Msaidizi na Katibu wa Magonjwa yasiyoambukiza, Dk. Joseph Mbatia, kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii alipata kusema kuwa, Serikali ipo mbioni kutengeneza sera itakayohusu utumiaji wa pombe ili kupunguza athari zake katika jamii.

Dk. Mbatia anasema wamelazimika kutunga sera hizo baada ya kuona matatizo yanayotokana na pombe yanaongezeka kila kukicha.
 Naye Daktari mstaafu, Maletnlema Tumsifu, anasema kuna madhara makubwa yanayosababishwa na unywaji wa pombe.
 Anayataja kuwa ni mfarakano katika familia, maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi, unene kupita kiasi, utapiamlo hasi, mimba kuharibika na kisukari.

Dk Maletnlema anasema yapo madhara ya aina mbili yanayotokana na pombe. “Kwanza ni kuathirika kwa mishipa ya fahamu mwilini kote kwa kupunguzwa uwezo na pili ni kuungua baadhi ya ogani za mwili hasa tumbo pindi mtu anapokunywa,” anasema

 Pia mtu akilewa kupita kiasi huwa hajijui na analala fofofo kutokana na kupoteza fahamu. Huenda akajikojolea au kutapika, inategemea na kiasi cha pombe alichokunywa.
 Wakati kwa upande wa mwili, pombe huathiri zaidi viungo vinavyopata pombe moja kwa moja mtu anywapo.

Mfano wa viungo hivyo ni mdomo, koo na tumbo, ambavyo vyenyewe hufikiwa na pombe moja kwa moja mara mtu anapomeza.

Kutokana na utaratibu wa tumboni, lazima chakula chote pamoja na sumu  au dawa vinavyonyonywa tumboni vipitie katika ini kuondoa sumu na vyakula visivyohitajika, hivyo basi ini huathiriwa kwa kiasi kikubwa.
  Sumu aina ya ethanol, iliyopo katika pombe kali, huchochea kwa kiasi kikubwa maradhi ya ini na saratani.

 Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Saratani (CIRF) inasema, asilimia 80 -85 ya pombe zinazotengenezwa Tanzania, hazina leseni.

Lakini pia, Tanzania haina sheria kubwa zenye nguvu kuhusu matumizi na uuzwaji wa pombe.
Sheria zilizopo ni ndogondogo ambazo huzuia uuzwaji wa pombe kwa watu wenye umri chini ya miaka 18 na ile ya kufunga baa ifikapo saa sita usiku. 
Udhaifu wa sheria za matumizi ya pombe, ndiyo unaochochea uwajibikaji mbovu, migogoro ya kifamilia na maradhi.

Nchi jirani ya Kenya, tayari wameweka sheria inayozuia uuzwaji wa pombe sehemu yoyote wakati wa kazi. Sheria hiyo ijulikanayo kama ‘Muthutho Law’ imeonyesha kufanikiwa kwa kiasi kikubwa na kudhibiti ulevi usio na tija. 

Chanzo: Mwananchi Jumapili