WAANDISHI wa habari wamekutana jijini Dar es Salaam na kuanza
mchakato wa kuunda mtandao utakaoweza kusimamia, kupigania na kutetea
haki zao.
Akizungumza katika kikao hicho juzi, Katibu wa muda, Ebenezer Mende,
alisema kuwa mtandao huo utajulikana kwa jina la ‘Waandishi wa Habari
Tanzania (TAJONET) na utakuwa wa nchi nzima.
Alisema mtandao huo utatumika kama chachu ya kusaidiana katika
matatizo mbalimbali, ukiwa na sauti moja katika kutetea maslahi yao na
utahusika moja kwa moja katika kusimamia maadili ya tasnia ya habari.
Mende alisema kuwa hatua hiyo imekuja baada ya wandishi wa habari
kujikuta wakikabiliwa na matatizo mbalimbali huku wakikosa msaada.
Aidha alibainisha kuwa TAJONET utakuwa bega kwa bega katika kuangalia
suala zima la afya ya wanachama kwa kuanzia ngazi ya chini kama matibabu
awapo hospitalini pamoja na misiba.
“Watu wengi wamekuwa wakichukulia matatizo ni kifo, bila kuangalia
mambo mengine kama ugonjwa, sisi hatutaki kujielekeza hivyo bali
tunataka tatizo la ugonjwa lipewe kipaumbele ili kuepusha vifo visivyo
na ulazima,” alisema Mende.
Alibainisha kuwa mkutano huo umeteua viongozi wa muda 14, ambao kati
yao wataunda kamati ya rasimu ya upatikanaji wa katiba ya mtandao huo.
Chanzo: Tanzania Daima |
|
|