Thursday, September 6, 2012

Mkurugenzi wa TCB aliyesimamishwa aendelea na kazi!



Licha ya Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba nchini (TCB), Marco Mtunga, kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili za kuwahujumu wakulima wa zao hilo, Mkurugenzi huyo bado anafanya kazi za bodi.

Mtunga alinukuliwa na gazeti moja la kila siku la lugha ya kiingereza siyo la Agosti 31, mwaka huu akiwasihi wakulima wa zao la pamba kukubali bei elekezi ya Sh. 660 iliyopangwa

Katika gazeti hilo,Mtunga alinukuliwa akisema: “Wakulima wetu wanapaswa wafahamu kuwa kushuka kwa bei ya pamba ni tatizo la kidunia, na TCB haitaweza kuongeza bei hiyo katika soko la Dunia, tumepanga bei hiyo kwa manufaa ya wakulima, ” alinukuliwa na gazeti hilo.

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alipoulizwa na NIPASHE sababu za Mtunga kuendelea na kazi wakati amesimamishwa, alijibu: “Katika sehemu ya barua aliyoandikiwa ya kusimamishwa kazi ilisomeka kuwa utakuwa nje kikazi, lakini ofisi ikikuhitaji kueleza jambo fulani utakuja kulitolea ufafanuzi.”

Chiza alisema kama Mtunga alinukuliwa na chombo cha habari akielezea suala fulani linalohusu sekta ya pamba hawezi kufahamu kama alipewa ruhusa au alijiamulia mwenyewe, hivyo aliomba muda wa kulifanyia utafiti suala hilo pamoja na kulisoma gazeti hilo kwa kuwa hakwepo nchini kwa muda mrefu.

“Naomba nilitafute hilo gazeti, nilisome kisha niwasiliane na Katibu Mkuu nijue sula la Mtunga limeishia wapi pamoja na hicho kitendo cha kuzungumza katika Media na nitalitoea ufafanuzi,” alisema Chiza.

Aidha Chiza alisikitishwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa kumtetea Mtunga kwa madai ya kuwa  ameonewa kusimamishwa kazi na makosa hayakuwa yake bali mkurugenzi aliyetangulia.

Chiza alimsimamisha Mtunga katika mkutano wa Nane wa Bunge na kusema uamuzi huo utasaidia uchunguzi huru wa tuhuma za uhujumu wa zao hilo zinazotolewa na wabunge.

Aidha waziri huyo alihaidi kumchukulia hatua za kisheria mkurugenzi huyo iwapo atakutwa na makosa yakiwemo ya kufuja fedha za fidia za wakulima wa pamba zilizotolewa mwaka 2009 na serikali na kusababisha zao hilo kushuka bei baada ya kuyumba kwa soko la dunia.

Tuhuma nyingine zinazomkabili Ntunga ni kushindwa kusimamia usambazaji wa dawa za kuua wadudu waharibifu wa pamba ambapo msimu huu dawa hizo hazikuua wadudu hali iliyoibua malalamiko kwa wakulima.

Ntunga alidaiwa kupitisha madai ya malipo ya Sh milioni 50 kwa kampuni itakayonunua zao hilo kwa kila kanda jambo lililopingwa kwa maelezo kwamba ni kumkandamiza mkulima kinyume cha uanzishwaji wa bodi hiyo.

Chanzo: Gazeti la Nipashe