Sunday, August 26, 2012

Zoezi la Kuhesabu watu na Makazi laanza Leo (sensa)



SENSA ya Watu na Makazi inaanza leo kote nchini na itadumu kwa siku saba, katika mpango unaotarajiwa kutoa takwimu za idadi ya watu na makazi utakaoisaidia Serikali kupanga uwiano wa kimaendeleo kulingana na maeneo nchini.

Sensa hiyo inafanyika huku Jeshi la Polisi likitoa onyo kali dhidi ya watu wachache waliojitokeza waziwazi kupinga mkakati huo kufanyika kwa ufanisi.

Hata hivyo, hadi jana jioni taarifa zilizopatikana kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, zinaonyesha hali kuwa shwari huku maofisa watakaosimamia mpango huo wakiwa kwenye harakati za mwisho za kuanza kazi hiyo.
Hata hivyo, Ofisa wa Uhamasishaji Sensa Taifa, Said Ameir aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa mpango wa sensa ulianza jana usiku jijini Dar es Salaam kwa kuchukua takwimu za watu kwenye maeneo wanayokaa watu wasio na makazi maalumu.

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni Uwanja wa Ndege, vituo vya mabasi na treni.

Alisema kuwa jana walikamilisha mkakati wa kugawa vifaa maeneo mengi nchini licha ya kuwepo matatizo ya hapa na pale kutokana na mawasiliano mabaya ya barabara.

Hata hivyo, Ameir alisema kuwa ingawa matangazo yanaonyesha sensa kufanyika kwa siku saba, lakini wameazimia kumaliza kazi hiyo ndani ya siku tatu au nne.

Kuhusu kuwapo baadhi ya watu na vikundi vinavyopinga sensa, Ofisa wa Uhamasishaji huyo alisema kuwa habari hizo wanazo lakini akasema watu hao ni wachache.

Hata hivyo, alisema kuwa ofisi yake itaendelea kuhamasisha ili watu wote washiriki sensa na kwamba anaamini watafanya hivyo.

"Ingawa wanasema ni Waislamu wote hawatashiriki, lakini hiyo siyo kweli, ni wachache. Mimi ni Mwislamu na nahamasisha watu wakiwamo Waislamu wenzangu washiriki sensa," alisema Ameir.

Wakati hayo yakiendelea, viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi, jana waliendelea kuhimiza watu kujiandaa kuhesabiwa kwa kuhakikisha wanajibu maswali yote ya makarani wa sensa kwa ufasaha.

Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar jana iliendelea kuwahimiza Wazanzibari kushiriki sensa kufuatia baadhi ya watu kutishia kususia zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika leo nchi nzima.

Baadhi ya wananchi wamesema kuwa watashirikiana na SMZ kuhakikisha sensa hiyo inafanikiwa, licha ya watu wengine kuanza kutoa vitisho kwa watakaoshiriki.

Songea
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Joseph Mkirikiti jana alikionya kikundi cha watu waliopanga kupita misikitini  kuzuia watu wasihesabiwe  akieleza kuwa watachukuliwa hatua kali.

Alisema kuwa ametoa kauli hiyo kutokana na taarifa za kuwapo kwa kikundi cha watu hao akiwataka wananchi wasikubali kuwasikiliza kwani nao watachukuliwa hatua za kisheria.