Friday, August 3, 2012

MCT yasikitishwa kufungiwa MwanaHalisi

http://mct.or.tz/mediacouncil/images/stories/Pixes/KubeneaSaed.jpg
Saed Kubenea akiongea na waandhi wa habari.

Baraza la Habari Tanzania (MCT), limesema limesikitishwa na kitendo cha kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi kwa kipindi kisicho na ukomo na kwamba haliungi kusimamishwa wala kufungiwa kwa chombo chochote cha habari kwa sababu yeyote ile.

Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mkajanga, alisema baraza linaamini makosa na matatizo ya kitaaluma hayawezi kumalizwa katika kufungia magazeti ama aina yeyote ya chombo cha habari.

“Kufunga ama kusimamisha vyombo vya habari ni ukiukwaji wa wazi wa uhuru wa vyombo vya habari kwa sababu kunawanyima wateja wa chombo hicho haki yao ya kupata habari za chaguo lao,” alisema.

“Kunawanyima raia ambao wamekuwa wakitumia chombo hicho haki ya kueleza maoni yao, kunanyima uhuru wa kujieleza na kukwaza demokrasia, hivyo kusimamishwa kwa gazeti la MwanaHalisi ni jambo la kusikitisha,” aliongeza.

Aidha MCT ilisema sheria ambayo serikali imeitumia kulifungia gazeti hilo ni ile ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wadau wa vyombo vya habari.