Monday, August 6, 2012

Leo ndio Mwisho wa uandikishaji vitambulisho Dar




Mamlaka ya Taifa ya Utambuzi (Nida),imesema haitaongeza muda kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kujiandikisha kupata vitambulisho vya Taifa na kusisitiza kuwa mwisho wa kujiandikisha ni leo.

Ofisa habari wa Nida, Thomas William, alisema hakutakuwa na muda wa nyongeza wa kujiandikisha kupata vitambulisho na kwamba na zoezi hilo litafungwa leo jioni.

Alisema wananchi wengi hawafiki katika vituo vya kujiandikisha siku za kazi, badala yake hujitokeza kwa wingi mwishoni mwa wiki.

“Tatizo la wananchi wanajitokeza mwishoni mwa wiki, hivyo tuliongeza muda wa wiki moja, lakini hatutaongeza tena siku hizo zitakapoisha,” alisema na kuongeza kuwa baada ya zoezi la uandikishaji kumalizika, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mtaa yenye watu sita, itazihakiki fomu hizo na kuzipeleka Nida.

Alisema baada ya fomu hizo kupelekwa Nida, zitahakikiwa tena na kuingizwa katika mfumo wa mtandao na nakala zake kutolewa na kurudishwa tena katika serikali za mitaa na kuhakikiwa tena na mjazaji fomu.

Alisema baada ya mjazaji fomu kuhakiki maelezo yaliyopo kwenye fomu hiyo kama  ni ya kwake na ni sahii, atachukuliwa alama za vidole pamoja na kupigwa picha tayari kwa zoezi la utoaji wa kitambulisho. 

Awali Nida ilipanga kukamilisha zoezi hilo mkoani Dar es Salaam Julai 30, lakini iliongeza wiki moja hadi leo ili watu wengi zaidi wajiandikishe.