Monday, August 13, 2012

Chuo cha IPS charuhusiwa kutoa elimu ya shahada

 http://www.nacte.go.tz/files/news/thumbnails/Seal%20of%20the%20Council_195x0.png

Chuo cha Ununuzi na Ugavi cha Chanika cha Dar es Salaam (IPS), kinatarajia kuanza kutoa elimu kwa ngazi ya shahada, baada ya kuruhusiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mtendaji wa NECTA, Primus Nkwera, katika mahojiano na MTANZANIA.

Alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya chuo hicho kuwa chini ya uangalizi wao kwa muda wa miaka mitano na kujiridhisha kwamba sasa kinafaa kutoa elimu kwa ngazi hiyo.

Alivitaja vigezo ambavyo wameviangalia hadi kukipa chuo hicho ithibati kuwa ni idadi ya walimu, wanafunzi wanaosajiliwa kila mwaka chuoni hapo na miundumbinu ya kuridhisha.

Alisema kwa mwaka huu wamekiruhusu kuchukua wanafunzi 100 kwanza kutokana na uwezo wa miundombinu iliyopo.

Akielezea kuhusu hali ya vyuo vingi vilivyopo chini yao kwa sasa, alisema si ya kuridhisha kwa kuwa vyuo vingi vilianza kazi kabla ya baraza hilo kuanzishwa.

Kutokana na hali hiyo, alisema wamekuwa wakikutana mara kwa mara na wamiliki wa vyuo na wale wanaoonekana kushindwa kujirekebisha kwa muda wanaopewa huwa wakiwafungia vyuo vyao.

Aliyataja majukumu ya baraza lao kuwa ni pamoja na kuvisaidia vyuo na kuwashauri wamiliki wake, kuishauri Serikali kuhusiana na masuala yanayohusu uendeshaji wa vyuo.

Alikiri kwamba kinachochangia vyuo vingi kuendeshwa pasipo kukidhi viwango kunatokana na ukosefu wa fedha.

Aidha, aliwataka wazazi kuwa makini wanapowapeleka watoto wao vyuo vikuu, kwa kuhakikisha vimesajiliwa na hatimaye wasijikute wamepoteza muda na fedha zao.

Kwa upande wa vyombo vya habari, alisema wapo katika mchakato wa kuhakikisha vyuo ambavyo havijasajiliwa havitangazwi kwa ajili ya kuepuka utapeli.

Alisema wana mpango wa kukaa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kuona ni namna gani sheria hiyo inaweza kupitishwa.

“Kwa kweli wamiliki wengine wamekuwa wakitafsiri jina la kusajiliwa na Serikali vibaya ukizingatia kwamba sisi ndio wasajili wakuu, lakini cha kushangaza utaona kwa siku vyuo sio chini ya vitano vinavyotangazwa katika televisheni sisi hatujawahi kuvisajili,” alisema Nkwera.

Chanzo: Mtanzania