Sunday, August 5, 2012

Barrick yafunga mgodi wa Bulyanhulu Kahama

https://encrypted-tbn2.google.com/images?q=tbn:ANd9GcQojzf9QpiLjy87OjCFu9M0J_nU5QfHq9Xv7m7nbFpafySRb512OQ


 Na Shija Felician, Kahama
 WAKATI sakata la kupinga sheria mpya ya mafao ya watumishi wanaoacha kazi katika sekta mbalimbali likizidi kushika kasi, Kampuni ya African Barrick Gold Mines juzi iliufunga mgodi wake wa Bulyanhulu baada ya wafanyakazi wake kugoma wakipinga sheria hiyo.

 Habari zilizopatikana katika mgodi huo mkubwa hapa nchini kwa uzalishaji wa madini ya dhahabu na shaba, zilieleza  kuwa chanzo cha kufungwa mgodi huo ni mgomo wa watumishi wanaofanya kazi ndani ya mashimo.

Hivi karibuni Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Mifuko ya Pensheni Nchini (SSRA), ilifanya marekebisho ya mafao ya watumishi wanaoacha kazi ama kufukuzwa kulipwa stahiki zao mpaka watakapofikisha umri wa miaka 55au  60 hatua ambayo ilipingwa na watu wengi.

Ofisa Uhusiano wa Kampuni hiyo Necta Foya,  alisema shughuli zote za uzalishaji zimefungwa kwa masaa 48 ingawa zile za utawala zinazofanyika  maeneo ya juu ya mgodi zinaendelea kama kawaida na baada ya muda huo watumishi wote waliosimama kazi wataitwa, na kwamba  watakaoonekana kukubaliana na masharti wataendelelea na kazi.

Kabla ya hapo uongozi wa mgodi huo uliwataka watumishi hao kuendelea na kazi  wakati suala lao likishughulikiwa baada ya kubaini wengi wao waliandika barua za kuacha kazi wakipinga masharti ya malipo ya ya pensheni .

Wafanyakazi  wanaofanya kazi shimoni ndio  wachimbaji wakuu wa madini  katika migodi ya aina hiyo wakisaidiwa na mafundi mitambo, na  hivyo kugoma kwao kufanya kazi kunaathiri uzalishaji kwa ujumla.

Hata  hivyo baadhi ya watumishi waliokumbwa na hali hiyo jana walikuwa wamezagaaa mjini Kahama wakionyesha wasiwasi wa kurudishwa kazini kutokana na mwajiri wao kuchukizwa na hali ya mgomo huo unaodaiwa kuisababishia hasara kampuni.

 Kwa mujibu wa Foya, leo wanatarajia kuongea na watumishi hao waliokuwa wamegoma baada ya masaa 48 kumalizika ambayo yalitolewa juzi wakati wa kufunga uzalishaji katika mgodi huo.