Sunday, July 8, 2012

Uongozi wa Soko la Mbagala walalamikiwa


Hili ni eneo maarufu huko mbagala.

WAFANYABIASHARA wa Soko Kuu la Mbagala jijini Dar es Salaam, wameutupia lawama uongozi wa soko hilo kwa kushindwa kufanya usafi katika soko hilo na hivyo kuhatarisha maisha ya wanaolitumia.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, juzi kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, Veronica Patrick, alisema licha ya soko hilo kutokuwa na miundombinu imara uongozi umeshindwa kutatua tatizo la uchafu ambalo sasa linaonekana kuota mizizi.
Alisema wafanyabiashara wa soko hilo hutozwa fedha za ushuru na manispaa kila siku wa sh 200 kwa wafanyabiashara wa kawaida na sh 300 kwa wenye maduka lakini uongozi umeshindwa kutatua kero ya uchafu.
“Ongezeko la baadhi ya matunda hasa machungwa limechangia mazingira ya soko kuharibika, hii imesababishwa na wafanyabiashara wenyewe kushindwa kujidhibiti lakini uongozi tunautupia lawama kwa kushindwa kuwajibika kwa sababu tunalipa ushuru kila kukicha, sasa unatumiwa kwa kazi gani?” alihoji.
Naye Katibu wa soko hilo, Frank Mapuli, alikiri kujitokeza kwa hali hiyo ingawa alisema imesababishwa na Manispaa ya Temeke kushindwa kushirikiana na uongozi wa soko hilo kuliboresha ikiwemo kumtafuta mzabuni kwa ajili ya usafi.
Mapuli alifafanua kuwa zaidi ya wafanyabiashara 1,200 kutoka ndani na nje ya jiji wanafanya biashara katika soko hilo, lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa miundombinu.