Tuesday, July 3, 2012

NHC Kuuza Nyumba kwa Bei Nafuu


SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) lina mpango wa kujenga nyumba 15,000 hadi ifikapo mwaka 2015 na kuziuza kwa bei nafuu kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Mkurungenzi Mkuu wa shirika hilo Nehemiah Mchechu alisema Jijini Dar es Salaam jana kuwa nyumba hizo zitaanza kuuzwa kati ya Sh25milioni hadi Sh40 milioni  kwa lengo la kumsaidia mwananchi wa kipato cha chini.

Baada ya kusaini mkopo wa Sh165 bilioni kutoka kwenye Taasisi tisa za kifedha,Mchechu alisema fedha hizi zitawasaidia katika mradi wa ujenzi wa nyumba na ununuzi wa ardhi ya akiba katika mikoa mbalimbali nchini.

“Nyumba tulizojenga zaidi ya 1,500 kwa mwaka huu  zimewalenga wananchi wa kipato cha chini yule ambaye atashindwa kununua nyumba ya Sh70,000 ataweza kununua nyumba za bei nafuu ambazo zitauzwa Sh25 hadi 40 milioni”alisema na kuongeza;

“Mradi huu wa ujenzi umeanza kutekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma ,Arusha na Dodoma huku miradi mingine ipo njiani kutekelezwa” alisema Mchechu

Pia alisema kati ya fedha hizo zilizotolewa  Sh23 bilioni zitapelekwa  kwenye ujenzi wa nyumba za bei nafuu ambazo nyumba hizo zitawalenga wananchi wa kipato cha chini.

Kwa upande wake  Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof Anna Tibaijuka alisema wananchi wametakiwa kununua nyumba badala ya kununua viwanja ili kuepuka gharama zisizokuwa na  msingi.

Waziri huyo alisema wananchi wataweza kukopa nyumba hizo ambazo mikopo yake italipwa kwa riba ya chini ili waweze kunufaika na mradi huo.

“Wananchi wanunue nyumba badala ya  kununua viwanja, hii  itamrahisishia kupunguza gharama ya kununua kiwanja na kujenga ambayo kiwango chake ni kikubwa”alisema Profesa Tibaijuka.
 Profesa Tibaijuka alisema kati ya nyumba hizo zinazojengwa asilimia 25 zitabaki kwa ajili ya watu ambao watahitaji kupanga.

Chanzo: Mwananchi