Friday, July 6, 2012

Mkuu wa Wilaya akataa chakula huko Bunda..


MKUU wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Joshua Mirumbe, amepiga marufuku wilaya hiyo kupokea chakula cha msaada kutoka Ghala la Chakula la Taifa kwa ajili ya wananchi badala yake walime kwa bidii.
Mirumbe alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata za Kabasa na Sazira wakati wa ziara yake ya kujitambulisha tangu ateuliwe kushika wadhifa huo.
Alisema wilaya hiyo inayo rutuba nzuri na yenye mabonde mengi yanayofaa kwa kilimo, hivyo ni vema wananchi wakayatumia mabonde hayo kwa ajili ya kulima mazao ya chakula kwa wingi waweze kuondokana na njaa.
Mirumbe alisema kuwa imejengeka tabia ya wananchi kutolima mazao ya chakula licha ya kuwa na maeneo hayo na badala yake wamekuwa wakitegemea chakula cha msaada kutoka serikalini ili wagawiwe, jambo ambalo alidai halitakuwapo tena katika wilaya hiyo.
Aliwataka wananchi kuacha kuzurura na kwenda kutembelea ndugu zao wakati wa kilimo na kwamba kila mtu mwenye uwezo wa kulima anatakiwa alime mazao ya chakula na biashara.
Mkuu huyo wa wilaya aliwaagiza maofisa ugani wa vijiji na kata kuhakikisha wanawasaidia wakulima kuwapa utaalamu ili waweze kulima kilimo chenye tija ambacho kitawakomboa.
Katika kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa, Mirumbe amepiga marufuku vijiwe vya kahawa, pombe za kienyeji, michezo ya meza, karata na kwamba mambo hayo yafanyike jioni baada ya saa za kazi