Saturday, June 23, 2012

Jiji lahakiki wafanyabiashara Wadogowadogo

MAMLAKA ya Jiji na Manispaa ya Ilala zinaendesha zoezi la uhakiki wa vizimba vya wafanyabiashara katika Soko la Machinga Complex ili kufahamu idadi ya wafanyabiashara halali.

Akizungumza na mwananchi jana,Mwenyekiti wa umoja wa wafanyabiashara sokoni hapo, Abubakari Rakeshi alisema, baada ya kuwa na uongozi mbovu kwa kipindi kirefu sasa hali imekuwa  shwari kwasababu mamlaka zinazohusika kama jiji wameanza kushughulikia suala la wanaomiliki wa vizimba zaidi ya kimoja.

Rakeshi alisema, kipindi cha nyuma kulikuwa na ubaguzi wa kupewa vizimba hasa katika vyama lakini sasahivi suala hilo limekwisha na kushauri kila mfanyabiashara amiliki kizimba kimoja tu.

“Kipindi cha nyuma mtu mmoja anaweza kumiliki vizimba zaidi ya saba lakini sasa hivi mtu akigundulika ana vizimba zaidi ya kimoja anapokonywa kwasababu sheria ni kuwa na kizimba kimoja”, alisema Rakeshi.

Alisema wafanyabiashara kwa sasa wameongezeka kutokana na kubomolewa kwa eneo la biashara la Shule ya Uhuru na hivyo kuwalazimu kuhamishia  mali zao katika soko hilo la Machinga.

“Karibu wafanyabiashara 88 wamehamia katika soko hili baada ya sehemu zao za biashara kuvunjwa”alisema Rakeshi.

Rakeshi alisema kwa sasa wateja wanaoenda kununua mahitaji katika soko hilo ni wachache hivyo alitoa wito kwa wateja kwenda sokoni hapo kwa wingi, kwani bidhaa zote zinapatikana.

“Kama unavyoona sasa hivi hadi simu,radio na kompyuta vinapatikana kama kariakoo vile”, alisema Rakeshi.

Aidha alitoa wito kwa wafanyabiashara wote kulipe kodi ili waweze kupata eneo la kituo cha magari katika eneo lao ambalo halina maegesho.

“Kodi za wafanyabishara zitasaidia kupata kituo cha mabasi na sehemu ya kuegesha magari,watu wengi wanashindwa kuja eneo hili kwasababu hakuna maegesho”, alisema.

Chanzo: Mwananchi