Monday, June 18, 2012

***BREAKING NEWS*** Mhariri wa Jambo Leo afariki ghafla Morogoro..

 

MHARIRI Mkuu wa gazeti la Jambo leo linalochapishwa na kampuni ya Jambo Concepts Limited, Willy Edward,  amefariki dunia usiku wa kuamkia jana katika mtaa wa Jumbe Mtoto eneo la Forest Manispaa ya Morogoro.
Taarifa za kifo chake zilizothibitishwa na jeshi la polisi mjini hapa na ambazo zimewashtua wengi zilieleza kuwa kifo cha mhariri huyo imetokea muda mfupi mara baada ya kupata chakula cha jioni na kuagana na watoto wake waliokuwa wakiishi na dada yake katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa mtoto wa dada yake, Catherine Rabani, kifo cha  mhariri huyo kilikuwa ni cha kushangaza sana hasa kutokana na madai kuwa mpaka anatoka nyumbani kwao majira ya saa 3.00 usiku marehemu alionekana kuwa na afya njema na wala hakuwa na dalili zozote za kuumwa.
Akielezea kutokea kwa kifo hicho, Rabani alisema kuwa marehemu baada ya kumaliza kula aliwaaga watoto wake na ndugu wengine kisha akatoka nje ambako dereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda alikuwa akimsubiri tayari kumrejesha katika hoteli aliyokuwa amefikia.
Alisema mhariri huyo mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam alikwenda mjini Morogoro Juni 16 kwa ajili ya kuhudhuria semina ya siku moja iliyokuwa imeandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.
Aliongeza kuwa mhariri huyo baada ya kufika nje ilipokuwapo bodaboda hiyo, ilidaiwa kuwa aliinama kidogo kisha akanyanyuka na moja kwa moja alianguka chali, hali iliyomlazimu dereva wa bodaboda kurudi ndani ili kutoa taarifa hiyo.
Alisema kuwa jitihada za kumuwahisha hospitali hazikuzaa matunda kwani baada ya kudondoka alipoteza maisha palepale na mwili wake ulipofikishwa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro majira hayo ya usiku ilionekana kuwa alikwishafariki dunia.
Baada ya kutokea kwa taarifa hiyo, waandishi wa habari jana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini, Azizi Abood, Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amir Nondo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Habari Corporation, Hussein Bashe walifika hospitalini hapo ili kuhakikisha kuwa mwili wa marehemu unasafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam.
Mwili wa marehemu huyo ulisafirishwa majira ya saa 6.00 mchana jana kwenda Dar es Salaam tayari kwa safari ya kwenda mkoani Mara kwa mazishi.