Monday, May 28, 2012

Hospitali ya Tumbi matatizo tupu

Maimuna Kubegeya, Kibaha

HOSPITAI ya Tumbi ya mjini Kibaha, Pwani, inayomilikiwa na Shirika la Elimu Kibaha, inakabiliwa na matatizo mbalimbali yanayoathiri utoaji wa  huduma wa wananchi.

Matatizo hayo ni pamoja na upungufu wa mashuka, mashine za kufulia na  upungufu wa damu hasa ikizingatiwa hospitali hiyo, ndiyo inayohudumia majeruhi wengi wa ajali za magari zinazotokea katika barabarani ya Dar es Salaam-Morogoro.

Hayo yalisemwa juzi na Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk Issach Lwali, alipokuwa akizungumza baada ya kupokea msaada wa mashuka 50, kutoka Kampuni ya Maxinsure ya jijini Dar es salaam.

Hafla hiyo ilifanyika katika Hospitali ya Tumbi, mjini Kibaha.

Dk Lwali alisema kwa sasa, hospitali hiyo ina jumla ya vitanda 250 lakini ina upungufu mkubwa wa shuka.

Alisema mwongozo wa wizara ya afya, unataka kila kitanda kutandikwa mashuka yasiyopungua nane kwa siku, lakini kwa sasa jambo hilo katika hospitali hiyo ya Mkoa wa Pwani, haliwezekani.
“ Kwa sasa hospitali yetu ina mashuka yapatayo 900 na hapo unaweza kuona ni kwa kiasi gani tuna uhitaji. Tuna uhitaji wa mashuka yasiyopungua 1,124. Kwa kweli tunafanya kazi katika mazingira magumu hasa ikizingatiwa kuwa tunapokea idadi kubwa ya wagonjwa,” alisema
Hospitali ya Tumbi kwa sasa inapokea wagonjwa kati ya 400 -700 kwa siku, wengi wao wakitokea Kibaha na Dar es salaam.
Dk Lwali alitaja tatizo lingine linaloikabili hospitali yake kuwa ni pamoja na ukosefu wa baadhi ya vipimo unaosababishwa na kukosekana kwa vitendanishi vya maabara.

Alisema hali hiyo imekuwa ikiulazimisha uongozi kuwashauri wagonjwa kuchukua vipimo katika hospitali nyingine, jambo ambalo alisema usumbufu mkubwa.
Ametaja baadhi ya vitendanishi vinavyokosekana kuwa  ni pamoja na vile vya kuchukulia vipimo vya wingi wa damu.

Kwa upande wa mashine za kufulia, mganga huyo amesema kwa sasa hali ni mbaya zaidi kwani wanatumia mashine moja tu ambayeo hata hivyo, haina uwezo mkubwa.
Akizungumza niaba ya Kampuni ya Maxinsure, Ofisa habari wa kampuni hiyo, Hamisa Juma, amesema wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kupata habari kupitia gazeti la The Citizen kuhusu matatizo yanayoikabili hospitali hiyo.
Ofisa habari huyo aliipongeza Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, kwa kuwa mstari wambele katika kuchapisha habari zenye maslahi kwa jamii ya Watanzania